Minister Esther Nasuwa: Msomi wa Biashara Anayeponya Familia Kupitia Table talk show
- Leo Nzali

- Jul 28
- 3 min read

Kutoka Benki hadi Madhabahuni:
Safari ya Wito wa Kuhudumia Familia
Kwa majina anafahamika kama Minister Esther Nasuwa, ambaye wengi humtambua kama Mama Mchungaji. Alimpokea Bwana Yesu Kristo mwaka 1989, akiwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shule ya sekondari. Tangu wakati huo alianza safari ya imani iliyomjenga kiroho na kumwandaa kwa huduma ambayo leo imekuwa baraka kwa familia nyingi.
Mbali na huduma yake kanisani, Minister Esther ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara (Master of Business Administration - MBA). Alifanya kazi kwa zaidi ya miaka 16 katika National Bank of Commerce (NBC) nchini Tanzania kabla ya kuhamia Marekani. Akiwa Marekani aliamua kubadili taaluma na kusomea Uuguzi (Nursing), na kwa sasa anafanya kazi kama Nurse.
Hata hivyo, taaluma yake haikuzima wito aliokuwa nao moyoni. Akiwa mke wa mchungaji na mama wa watoto wawili, Derick na David, aliendelea kuona maumivu ya familia nyingi zilizokuwa zikivunjika na vijana waliokuwa wakikosa mwongozo sahihi. Hapo ndipo alipoanza kutambua kuwa Mungu alikuwa amemkusudia kuwa sauti ya matumaini kwa familia nyingi.
Family Today Table Talk Show:
Jukwaa la Kurejesha Amani Katika Familia
Kutokana na mzigo huo wa kiroho, Minister Esther Nasuwa alianzisha kipindi cha Family Today Table Talk Show, jukwaa linalolenga kutoa elimu, ushauri na mwongozo kuhusu ndoa, malezi ya watoto na changamoto zinazowakabili vijana katika kizazi cha sasa.
Anasema licha ya kuwa ni muuguzi, amekuwa akijifunza kwa kina kupitia wataalamu wa saikolojia ili kuelewa tabia za binadamu na changamoto za mahusiano.
"Ninasoma Nursing, lakini ninawasikiliza psychologists wengi wanaozungumzia tabia mbalimbali za watu na changamoto nyingi za mahusiano zinazotokana na tabia hizo."
Kwa mujibu wake, uzoefu wa kuwa mke wa mchungaji umemsaidia sana kuelewa mahitaji ya familia nyingi.
"Ukiwa mke wa mchungaji unakuwa mama wa familia nyingi. Sio familia yako tu. Changamoto za watoto, ndoa na hata magonjwa zinakuwa sehemu ya maisha yenu. Hapo ndipo Mungu amenipa nafasi ya kuendelea kuitumia huduma aliyoweka ndani yangu."
Kupitia kipindi hicho, amekuwa akiwasaidia wanandoa, wazazi na vijana kupata mwanga wa kibiblia na wa kitaalamu kuhusu namna ya kujenga familia imara zenye upendo, heshima na mawasiliano mazuri.

Changamoto za Kizazi cha Leo:
Wito wa Kujenga Familia Zenye Amani
Minister Ester anaamini kuwa familia nyingi za kizazi cha sasa zinakabiliwa na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya maisha ya kisasa.
"Siku hizi changamoto kubwa ni utandawazi. Watu wanajilinganisha sana na wengine. Hata suala la cheating limeongezeka, si tu kimwili bali hata emotional cheating kupitia simu na mitandao ya kijamii."
Anaongeza kuwa hata familia za Kikristo zimeathirika kwa sababu baadhi ya waumini hawaishi maisha yanayofanana na mafundisho ya Kristo.
"Zaidi ya asilimia 50 ya ndoa za Kikristo zinaishia kwenye talaka kwa sababu Wakristo wengi hawaishi maisha ya Kristo wala kufuata mfano wake."
Kwa familia za Watanzania na Waafrika wanaoishi diaspora, Minister Esther anatoa wito wa kuweka amani mbele ya kila jambo.
"Ningependa kuzihimiza familia zote kujenga nyumba zenye upendo, umoja na amani. Neno la Mungu linasema palipo na umoja ndipo Mungu huamuru baraka. Baraka hizo si fedha pekee, bali pia afya njema, watoto kufanikiwa, ukuaji wa kiroho na hata kuona wajukuu na vitukuu vyetu."
Anamalizia kwa kusisitiza kwamba mafanikio ya kweli hayawezi kujengwa juu ya maumivu ya familia.
"Huwezi kufanikiwa huku ukimuacha mwenzi wako analia au watoto wako hawana amani. Hata kama utafanikiwa, mafanikio hayo hayatadumu. Familia yenye amani ndiyo msingi wa baraka za Mungu."

Kupitia Family Today Table Talk Show, Minister Esther Nasuwa ameendelea kuwa sauti yenye matumaini kwa familia nyingi ndani na nje ya Afrika. Safari yake kutoka kwenye sekta ya benki, kupitia taaluma ya uuguzi hadi huduma ya malezi ya familia, inaonyesha kwamba wito wa Mungu unaweza kutimizwa kupitia taaluma yoyote.
Katika wakati ambapo familia nyingi zinapitia changamoto za utandawazi, mabadiliko ya maadili na migogoro ya mahusiano, huduma yake imekuwa daraja la kurejesha mawasiliano, upendo na msingi wa Kikristo ndani ya nyumba nyingi. Ujumbe wake unabaki kuwa mmoja: Familia yenye amani ndiyo urithi mkubwa zaidi ambao wazazi wanaweza kuuacha kwa watoto wao na vizazi vijavyo.










Comments